MKUTANO WA 58 WA KAMISHENI KUHUSU HALI YA WANAWAKE
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi. Anna T. Maembe akisisita haja na umuhimu wa
wazazi kuwawezesha watoto wao wa kike kuyapenda masomo ya sayansi, teknolojia,
uhandisi na hesabu ( STEM) badala ya kuliachia jukumu hilo serikali au walimu.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa pembezoni ulioandaliwa kwa pamoja kati ya
Tanzania, Uingereza na Kampuni ya Kimataifa ya GlaxoSmithkline ili kujadili
fursa na changamoto za mwanafunzi wa kike katika masomo hayo, kulia kwa Katibu
Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bibi. Irina Bokova ambaye alikuwa modereta wa
majadiliano hayo na pia alielezea nafasi na Mchango wa UNESCO katika kumsaidia
mtoto wa kike. Kushoto ni Balozi Ramadhan Mwinyi , Naibu Muwakilishi wa Kudumu
wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Wizara ya Wanawake na Usawa
wa Uingereza, Bibi, Maria Miller ( Mb) akielezea uzoefu wa nchi yake katika
kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya STEM, kulia kwake ni Bibi Nicola
Yates, Makamu wa Rais wa UK and Ireland Phamarceuticals na Meneja Mkuu wa
GlaxoSmithkline. Nyuma ya Waziri Miller na anayefuatilia kwa makini majadiliano
hayo ni Mwanamitindo Bi. Flaviana Matata ambaye pamoja na kujikita fani ya
mitindo na ambayo imemjengea heshima kubwa, lakini pia kupitia Taasisi yake ya
Flaviana Matata Foundation ameonyesha mapenzi makubwa ya kuwasaidia wanafunzi
kuipenda shule na kudumu shuleni.
sehemu wa washiriki wa Mkutano wa 58 wa
Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, walioshiriki majadiliano hayo ambapo pia
walipata fursa ya kuchangia kwa kuuliza maswali meza kuu iliyowahusisha Katibu
Mkuu, Anna Maembe, Mkurugenzi Mkuu UNESCO, Irina Bokova, Waziri Maria Miller (
Mb) na Nicola Yates Meneja Mkuu GlaxoSmithkline ambao ndio waliokuwa
wazungumzaji wakuu.
Katibu Mkuu Maembe akipeana mkono na
Waziri Miller ( Mb) mwishoni mwa mkutano huo wa pembezoni.
Tatizo la wanafunzi wa kike
kutochangamkia au kuyapenda masomo ya sayansi, teknolojia,
uhandisi na hisabati (STEM) ni tatizo linalozikumba nchini
nyingi duniani zikiwamo zilizoendelea.
Na kwa sababu hiyo imeelezwa
kwamba, ushirikiano wa karibu kati ya serikali kuu, sekta binafsi,
wazazi , walimu na wanafunzi wa kike unahitajika hivi sasa
kuliko wakati mwingine wowote na hasa wakati huu ambapo
Jumuiya ya kimataifa inajipanga na kuandaa ajenda mpya za
malengo ya maendeleo endelevu baada ya 2015.
Hayo yamejitokeza siku ya jumatano
wakati wa mkutano wa pembezoni ulioandaliwa kwa pamoja kati
ya Tanzania, Uingereza na Kampuni ya Kimataifa ya
GlaxoSmithkline na kuwashirikisha wajumbe wanaohudhuria mkutano
wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake unaoendelea hapa Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu, kutoka Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsai, Bibi Anna Maembe kwa
upande wa Tanzania, Bibi Maria Miller ( Mb) Waziri wa Wanawake na
Usawa kwa upande na Uingereza na Bibi. Nicola Yates Makamu wa Rais
wa Kampuni ya Kimataifa ya Madawa ya Uingereza na Ireland na
Meneja Mkuu wa GlaxoSmithkline ndio waliokuwa wazungumzaji wakuu wa
mkutano huo ambao dhumuni lake lilikuwa ni kutafakari,
kubadilisna uzoefu, changamoto na kutafuta mbinu zaidi za kuwasaidia
wanafunzi wa kike kupenda STEM.
Mkutano huo ambao ulivutia washiriki
wengi hadi wengine kukosa nafasi ya kuingia, modereta wake alikuwa
ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Bibi. Irina Bokova.
Akielezea uzoefu wa Tanzania na
changamoto zake katika eneo hilo , Katibu Mkuu Anna Maembe, amesema,
pamoja na kwamba serikali kuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo
sekta binafsi kuweka mifumo mbalimbali inayolenga kuwasaidia na kuwahamasisha
watoto wa kike kuchangamkia masomo hayo bado safari ni ndefu.
Akasema changamoto kubwa ni katika eneo
la ufuatiliaji ili kubaini kama wanafunzi waliosaidiwa na kujengewa uwezo
wamefikia wapi katika masomo yao na baada ya kuhitimu je wanafanya kile
walichosomea.
Akaongeza kuwa itakuwa ni kazi
bure kama serikali peke yake itaachiwa jukumu hilo pasipo wazizi wenyewe
kuhamasika na kuwajengea mazingira mazuri watoto wao wakike tangu wakiwa
na umri mdogo wa kuyapenda masomo hayo.
“Sisi katika Tanzania
tunaishukuru sana serikali kwa mchango wake wa kuwasaidia wanafunzi wa
kike kujiunga na masomo ya sayansi, hesabu, uhandisi na teknolojia,
lakini serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu, nafasi ya
wazazi ni muhimu sana sana” akasisitiza.
Akaongeza pia kuwa Tanzania
inao wanawake ambao ni wahandisi, wataalamu waliobobea katika ufundishaji
wa hesabu, sayansi na hata utafiti na wengine wanaongoza
Idara za Serikali au kampuni binafasi.
Akasema hao wote wanaowajibu wa
kujitokeza ili kutumia uzoefu wao kuwahamasisha wanafunzi wa kike kufikia pale
walipofika wao.
Naye Waziri wa Uingereza yeye
alisema, hata katika nchi yake, bado wanafunzi wengi wa kike hawapendi
masomo hayo, na hata kama wakiyasoma, si wote waoishia kufanya kazi
walizosomea.
Akasisitiza haja na umuhimu wa sekta
binafsi kusaidiana na serikali katika eneo hilo na pia
umuhimu wa watoto wa kike kuhamasishwa na kujengewa uwezo wakiwa wangali
wadogo ili kutambua vipaji vyao.
Naye Makamu Rais na
Meneja Mkuu wa GlaxoSmithKline yeye aliainisha program mbalimbali
ambazo kama sekta binafsi imekuwa ikichangi katika eneo hilo.
Akasema uzoefu uonyesha kuwa
watoto wa kike wakiwezeshwa na kuhamasishwa wakiwa wangali wadogo
wanayofursa kubwa ya kupenda hesabu, sayansi, uhandisi na masuala ya
teknolojia. Na pia inakuwa hamasa kwao wakiwaona wanawake waliofanikiwa katika
maeneo hayo.
Na Mwandishi Maalum
No comments:
Post a Comment