BALOZI
MONGELLA ATUNUKIWA TUZO YA UMAHIRI AFRIKA
waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba amemkabidhi tuzo ya
umahiri katika uongozi Mhe Balozi Getrude Mongella kutokana na juhudi zake
katika kuwakomboa wanawake wa Bara la Afrika.
Hafla ya
kukabidhi Tuzo hiyo ya miaka 50 ya Pan African Women’s Organization (PAWO)
ilimefanyika leo (23/12/2013) Courtyard Hotel jijini Dar es salaam na
kuhudhuriwa na Viongozi wa Wizara waliongozwa na Katibu Mkuu Bibi Anna T.
Maembe na kushirikisha wajukuu wa Balozi Mongela.
Mhe. Sophia Simba
alifafanua kuwa lengo la hafla hiyo ni kutambua utumishi wake na kumkabidhi
Mheshimiwa Mongella Tuzo ya heshima ya Wanawake Mashuhuri Barani Afrika ambao
walionesha uongozi uliotukuka katika kutetea umoja, haki na usawa wa wanawake.
Awali tuzo hiyo ilitolewa katika Mkutano maalumu wa Mawaziri wa Wanawake na
Jinsia uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini mwezi Agosti 2-13, 2013.
Aidha, Wizara imetambua umuhimu wa kujulisha taifa kuhusu mchango wa Balozi
Mongella na kutokana na uzoefu wake uliosaidia ukombozi wa wanawake wa Barani
Afrika. Itakumbukwa
kuwa Mhe. Mongella alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa Wanawake uliofanyika
Beijing Nchini China mwaka 1995. Matokeo
ya Mkutano huo ni maandalizi ya Azimio na Ulingo wa Beijing, ambao uliainisha
maeneo 12 ya kimkakati ambayo utekelezaji wake umesaidia kuleta usawa wa
kijinsia na wanawake kupatiwa haki zao.
Nchi ya Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatekeleza maeneo hayo
muhimu ikiwa ni pamoja na elimu na mafunzo, afya, ajira, uwezeshaji kiuchumi,
usawa, kushiriki uongozi na maamuzi na kuzuia ukatili wa kijinsia nk.
Akiwa Rais wa Bunge la Afrika Mhe. Mongella alitumia nafasi
hiyo kuelimisha na kutetea maslahi ya wanawake Barani Afrika. Aidha, amekuwa
akishiriki kikamilifu katika mikutano mbalimbali inayohusu maendeleo ya
Wanawake na jinsia katika ngazi ya kikanda. Katika ngazi ya kitaifa Mheshimiwa
Mongela ametumikia nyadhifa mbalimbali kama vile Waziri, Mbunge, na amekuwa
mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wanawake hapa nchini.
Simba alisisitiza kuwa Mheshimiwa
Mongella amesimama kidete kutetea maslahi ya wanawake, jambo ambalo linamfanya
kuwa mfano wa kuingwa na wanawake wote wa kitanzania maana ametenda kwa uthabiti na leo
tunajivunia uzoefu wake.
Akitoa shukurani zake
Mheshimiwa Balozi Mongella alikumbusha kuwa chanzo cha kuanzishwa kwa Pan
African Women’s Organization ni Tanzania (PAWO). Na kwamba ilianza mapema hata
kabla ya kuanzishwa kwa vuguvugu la Umoja wa Nchi za Afrika (OAU). Changamoto
kubwa ni kwamba kutothamini ubunifu wetu wenyewe kumesababisha PAWO kulegalega.
Hafla hii inatukumbusha kuthamini michango ya wazalendo ili kusisimus fikra
zenye manufaa katika jamii.
Njozi ya Balozi Mongella ni kuona
kuwa watoto wa kike wanapatiwa haki ya elimu ili kuzalisha akina -Mongella
wengi nchini. Aidha, vijana wameaaswa kuwa na maadili na kuepuka matusi ya
waziwazi katika kutafuta nafasi za uongozi jambo linalovunja heshima na utu.

No comments:
Post a Comment