KATIBU MKUU WIZARA
YA MAENDELEO YA JAMII AKEMEA DAWA ZA KULEVYA, ASEMA WATANZANIA ZAIDI YA 500
WASHIKILIWA NCHI ZA NJE, WENGINE 100 WASUBIRI KUNYONGWA NCHINI CHINA
KATIBU Mkuu wa wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto Anna
Maembe amewataka vijana nchini kuachana kabisa na biashara ya dawa za kulevya
kwani inawasababishia matatizo makubwa katika maisha yao badala yake wajiunge
na kutengeneza vikundi vya kijasiriamali ili serikali iweze kuwasaidia
kujikwamua kimaisha na kufikia ndoto zao.
Amesema takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa, zaidi ya vijana
500 wa Kitanzania wako kizuizini katika nchini tofauti duniani walikokamatwa
wakisafirisha dawa hizo, huku vijana wengine wapatao 100 wakiwa wamehukumiwa
kunyongwa nchini China.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya
kijamii wakati wa ziara yake katika kata ya Matai wilayani Kalambo Mkoa wa
Rukwa jana, ambapo alisema biashara hiyo inachafua sana jina la Tanzania katika
Jumuia ya Kimataifa kutokana na idadi kubwa ya vijana kujihusisha na biashara
hiyo.
Akizungumzia sera ya Jinsia inayotekelezwa na wizara yake, Katibu
Mkuu huyo alisema haina lengo la kuwafanya wanawake kuwatunishia misuli wanaume
katika familia bali ni kuwawezesha wanawake kushiriki katika uzalisha na kukuza
kipato cha familia na taifa kwa ujumla ili kukabiliana na gharama za
maisha ambazo zimepanda sana kwa sasa.
Vilevile alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanatenga muda wa
kukaa na kuzungumza na watoto ili kujua changamoto zinazowakabili ikiwemo
unyanyasaji wa kijinsi na kisaikolojia wanazokumbana nazo na pia kuwapatia haki
zao za kimsingi kama elimu, afya na kusikilizwa kama ambavyo sera ya
watoto hapa nchini inavyoelekeza.
Katika kuimarisha vikundi vya wanawake mkoani Rukwa, katibu mkuu
Maembe ametoa shilingi milioni 43 kutoka katika wizara yake, ambapo vikundi
kutoka katika Halmashauri za wilaya ya Nkasi, Kalambo, Sumbawanga Vijijini na
Manispaa vitanufaika kwa mtindo wa wanachama wa vikundi hivyo kupatiwa mikopo
kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.

No comments:
Post a Comment