TAARIFA
YA WIZARA KULAANI MATUKIO YA MAUAJI YA
KIKATILI YA WANAWAKE KATIKA WILAYA YA BUTIAMA
MKOA WA MARA
Hivi karibuni kumekuwa na
taarifa za kutisha katika Wilaya ya Butiama mkoa wa Mara ambapo imearifiwa baadhi
ya wanawake kuuawa kikatili kwa kukatwa vichwa. Sababu ambazo hazijathibitishwa
zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni pamoja na imani za kishirikina, uchu
wa kumiliki mali, kulipiza visasi na kuendekeza hulka ya ukatili kwa kudhani
kuwa mhusika anapata heshima yoyote katika jamii.
Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuwepo kwa
mauaji hayo ya kikatili na inawataka wananchi kutoa ushirikiano thabiti ili kuhakikisha
kuwa matukio hayo ya udhalimu YANAKOMA MARA
MOJA.
Wizara inalaani vikali mauaji ya wanawake waliokatishwa
maisha yao kutokana na kuuawa na watu wenye fikra potofu dhidi ya wanawake.
Wizara inasisitiza kwamba wanawake wanayo haki
ya kuishi kama inavyosisitizwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayotamka
kuwa ‘Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na
kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa Mujibu wa Sheria.’
Wakati mwingine wanawake wamekuwa
wakikandamizwa katika jamii kutokana na tofauti za kimaumbile na hivyo kusababisha
ukatili au mauaji. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya
kuthaminiwa utu wao na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao
unaweza kuhatarisha haki zao ikiwemo haki ya kuishi ambayo ndio haki kuu kuliko
haki zote.
Vitendo vya mauaji ya kikatili
wanavyofanyiwa wanawake wa wilaya ya Butiama ni jambo ambalo linasababisha hofu
kubwa miongoni mwa wanawake. Mauaji hayo yana wakosesha amani na utulivu na
hivyo kuzorotesha ari yao katika shughuli za uzalishaji mali kwa wanawake wa wilaya ya Butiama na Taifa kwa ujumla. Mwananchi ambaye anawindwa kama mnyama kamwe hawezi
akashiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa kuogopa kuwa, maisha yake yako hatarini.
Kwa kutambua hili Wizara inaagiza
wadau wote kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha kwamba uhai wa wanawake wa
Butiama na kote nchini unalindwa. Wananchi watambue kuwa tukio la
mauaji dhidi ya mtu yeyote ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa la jinai.
Katika
kipindi hiki cha majonzi, Wizara inatoa pole kwa familia ambazo zimeguswa na mauaji
ya ndugu zao waliopoteza maisha, Wizara
inahimiza wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji
wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua ili kukomesha tabia hiyo.
Mwisho, Wizara inapenda kuikumbusha jamii kuwa, mauaji ya
kikatili dhidi ya wanawake yanapingana na jitihada kubwa za Taifa katika
kutekeleza sheria za nchi na Mikataba ya
Kimataifa na Kikanda kuhusu haki na usawa wa kijinsia,
Aidha ni
wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanaishi katika
hali ya usalama, amani na utulivu.

No comments:
Post a Comment