JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU
YA WANAWAKE DUNIANI TAREHE 8 MACHI, 2014
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU WIZARA YA
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 8
Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Madhumuni ya maadhimisho haya ni
kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya
Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na
usawa wa jinsia.
Madhumuni mahususi ya kuadhimisha Siku ya
Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa
wanawake katika kuchangia kuleta maendeleo yao endelevu; kuelimisha jamii
kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau katika kuwajengea
uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea
maendeleo yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2014 ni: ”Chochea
Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia”. Ujumbe huu unasisitiza
kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia
katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo. Mwelekeo wa maendeleo kijamii, kitaifa na kimataifa unasisitiza na
kuhimiza kuandaa na kutekeleza mipango inayozingatia ushirikishwaji na ushiriki
stahiki wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2014 yatafanyika ngazi ya mkoa. Maadhimisho hutoa
fursa maalum kwa Taifa, mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio
yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke na kubainisha changamoto zinazowakwamisha
kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na kuweka mikakati ya
kukabiliana na changamoto hizo.
Wizara ya Maendeleleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatoa wito kwa mikoa yote
kushirikisha wananchi na wadau wote katika kuadhimisha siku hii kwa namna
watakavyoona inafaa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu. Kwa pamoja tunaweza
kushiriki kujiletea maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla. Nimatumaini yangu
kuwa kupitia maadhimisho haya jamii itachochea mabadiliko ya kuwashirikisha
wanawake na wasichana katika kupanga na kutekeleza mipango mkakati na progamu
za kiuchumi, kijamii na kisiasa ili
kufikia maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Aidha, nawaomba wanahabari wote nchini kushirikiana na wadau mbalimbali
ikiwemo Serikali na taasisi zisizo za kiserikali, asasi za kiraia na wadau wamaendeleo
kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha jinsi mwanamke na
msichana akipewa fursa na kuwezeshwa hutoa mchango mkubwa sana kwa familia yake
na taifa kwa ujumla. Hili ndilo lengo la kuadhimisha siku hii. Tueleweke kuwa
wanawake ni zaidi ya asilimia 50 (hamsini) ya watanzania wote.Wakishirikishwa
ipasavyo katikia shughuli za maendeleo mchango wao ni mkubwa sana.
Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
03/03/2024
No comments:
Post a Comment